ANGALIA MKE WA MTU ADAI KURUHUSIWA KUZAA NJE YA NDOA, AFANYA KWELI

Bofya Hapa

NI aibu nzito! Mwanamke mmoja, Esta Msomi (26) (pichani), mkazi wa Kijiji cha Mwibagi kilichopo katika Kata ya Kyanyari Wilaya ya Butiama mkoani Mara, ametoa kali ya mwaka baada ya kudai kuwa aliruhusiwa na mumewe kuzaa nje ya ndoa na alipofanya hivyo, amemtishia maisha na kumtelekezea watoto.

Mwanamke huyo amedai kuwa mumewe aitwaye Chacha Wambura (32) amekuwa akimfanyia vitisho hivyo huku akimpiga na kumfukuza nyumbani mara kwa mara na sasa anaishi kwa tabu baada ya kutelekezewa watoto. Akielezea juu ya kutelekezwa na kutishiwa maisha, mwanamke huyo ambaye kwa sasa anaishi nyumbani kwao Kiabakari, alisema mumewe amekuwa akifanya hayo baada ya kuoa mke mwingine mapema mwaka huu ambapo sasa maelewano ndani ya nyumba yaliisha na amekuwa akimnyanyasa na kumpiga huku akimtolea matusi kwamba aondoke hapo nyumbani na aende popote kwa sababu amemfilisi mali zake nyingi tangu amuoe miaka 16 iliyopita

. Esta alidai kuwa, Machi 17, mwaka huu majira ya saa 6.00 mchana alishangaa kumuona mumewe akiingia ndani na panga alimokuwa akifanya shughuli zake za maandalizi ya chakula cha mchana na akamtishia maisha. Alidai kuwa siku hiyo yalitokea mabishano makali kati yake na mumewe na alipigwa lakini alipata nafasi akakimbia huku akipiga kelele zilizofanya umati kufurika hapo nyumbani kumpa msaada. Mume.

Alifafanua kwamba, kutokana na kitendo hicho aliondoka nyumbani kwake na kwenda kuishi kwao Kyabakari na baadaye kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Kiabakari ambako alipewa barua ya wito akampe mumewe ili afike kituo cha polisi lakini baada ya kupewa barua hiyo na mwenyekiti wa kitongoji, mume huyo aligoma kwenda kituoni hapo. Baadaye mwanamke huyo alirudi tena kituo cha polisi na kupewa ushauri wa kwenda Mahakama ya Mwanzo Kukirango ili adai haki zake za msingi pamoja na talaka yake.

Aidha, Esta alieleza kuwa, tangu mumewe amfukuze nyumbani kwake Machi 17, mwaka huu watoto wake wawili wanaosoma aliondoka nao na hawasomi kwani walikuwa wakisoma Shule ya Msingi Terita iliyopo katika Kijiji cha Mwibagi, mmoja akiwa darasa la tatu na mwingine darasa la pili wakati mtoto wa tatu ana umri wa miaka mitatu na nusu.

Hata hivyo, mumewe huyo alipoulizwa juu ya tuhuma hizo za mkewe alikiri kuoa mke wa pili na akasema chanzo cha yeye kuamua kuoa tena na kumfukuza mkewe mkubwa ni baada ya mkewe huyo kumsaliti na kuzaa mtoto nje ya ndoa yao miongoni mwa hao watoto wao watatu. “Licha ya kuzaa nje ya ndoa, mke huyo amepata ujauzito mwingine nje ya ndoa ambao hadi sasa anao, sikuvumilia, nikamtimua,” alisema mume huyo.

Uwazi lilimrudia mke na alipoambiwa kwamba kuna madai ya yeye kuzaa nje ya ndoa, alikiri na akadai kuwa mumewe ndiye aliyempa ruhusa ya kuzaa nje ya ndoa tangu mwaka 2010, baada ya kumruhusu kuwa atafute mume nje mwenye afya njema awe anazaa naye.

Aliniambia nizae nje ya ndoa na yeye atakuwa anawatunza watoto hao kama wa kwake wa kuzaa, lakini nashangaa baada tu ya kuoa mke mwingine anaamua kunitishia maisha na kunifukuza,” alidai mama huyo. Stori: GREGORY NYANKAIRA, Mara