BREAKING : MAFURIKO YAUWA WAUU 5,NI MAJANGA WENGINE WAPIGWA NA RADI

Bofya Hapa

WATU watano wamepoteza maisha wakiwamo ndugu wawili ndani ya siku tatu katika matukio ya kufa maji katika mvua za mafuriko wilaya za Handeni na Lushoto mkoani Tanga. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe, jana alithibitisha kutokea kwa vifo vinne vilivyotokana na mafuriko na cha mtu mmoja aliyepigwa na radi. Bukombe alisema Jumamosi saa 10 jioni wilayani Lushoto watu wawili ambao ni ndugu, Kassim Yahaya na Awadh Yahaya, wakazi wa Kitongoji cha Mbugui Chini walikufa maji wakivuka mto Lukundo. Naye Mwamini Ally (46), mkazi wa Kijiji cha Rangwi alikufa kwa kusombwa na maji ya mto Ngurumo.

Tukio lingine lilitokea Ijumaa jioni katika Kijiji cha Zavuza Kata ya Kiva wilayani Handeni ambapo Mwanahawa Rajab (60) alikufa kwa kusombwa na maji katika bonde la Bangala na Shaban Juma (30), mkazi wa Kijiji cha Mwamgodi Kata ya Msasa wilayani humo alikufa kwa kupigwa na radi. Hata hivyo, alisema marehemu hao walikufa baada ya kuzidiwa nguvu na maji hayo na kuwasomba na miili iliopolewa na kuzikwa kwenye vijiji vyao baada ya taratibu zote za kiuchunguzi kukamilika.

Bukombe aliwataka wananchi wachukue tahadhari wanapovuka mito na kuwalinda watoto hasa kipindi hiki ambacho mvua zinazoambatana na upepo zikiendelea ili kujiepusha na majanga ambayo yanaweza kuepukika. Katika hatua nyingine, Kamanda Bukombe alisema watu watano wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walivamia nyumba ya mfanyabiashara Allen Daud, mkazi wa mtaa wa Magaoni jijini Tanga na kupora zaidi ya Sh. milioni 7 baada ya kuwafunga kamba waliokuwamo.

Bukombe alieleza tukio hilo lilitokea Ijumaa mchana, baada ya watu hao ambao mmoja wao akiwa amevalia sare za polisi kuwapora kiasi hicho cha pesa na simu mbili na laptop moja na kutoweka. “Watu hao moja akiwa amevalia sare za polisi wakitumia gari aina ya Rav 4 namba T 764 CKD walifika nyumbani hapo na kujitambulisha kama askari, ghafla waliwaweka chini ya ulinzi watu watatu waliokuwapo na kuwafunga kamba miguuni na plasta midomoni na kuwapora kabla ya kutoweka,” alisema Bukombe.

Alisema msako wa polisi ulifanikiwa kulikamata gari hilo eneo la Kabuku Wilayani Handeni ambapo watu wawili kati ya watano waliyokuwamo walifanikiwa kutoroka na vitu vilivyokutwa ndani ya gari hiyo ni saremoja ya polisi, bastola bandia moja, redio call, vipande viwili vya nondo, panga, simu moja ya mlalamikaji na zaidi ya Sh. 700,000. Bukombe aliwataja watu watatu waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ambao walikuwa kwenye gari hilo kuwa ni Msafiri William (32), mkazi wa Gongo la Mboto, Rashid Yussuph (29), mkazi wa Temeke na Rashid Shaibu (25) mkazi wa Keko jijini Dar es Salaam