LUPITA NYONG’O ASINGEIGIZA ANGEFANYA KAZI YA MASAJI!

Bofya Hapa
Actress Lupita Nyong'o, of the film "12 Years A Slave," arrives at the 71st annual Golden Globe Awards in Beverly Hills, California January 12, 2014. REUTERS/Mario Anzuoni (UNITED STATES - Tags: ENTERTAINMENT) (GOLDENGLOBES-ARRIVALS) - RTX17B4R

NIKIWA binti mdogo mama yangu aliwahi kuniambia kwamba, uzuri hauliwi na hauwezi kumletea mtu yoyote mabadiliko katika maisha. “Kinachoweza kumletea mabadiliko mtu ni kujiamini na kuamini kile alichobarikiwa na Mungu.” Hayo ni maneno ya muigizaji maarufu duniani kwa sasa Lupita Nyong’o, wakati akizungumza na mamilioni ya watu duniani waliokuwa wakifuatilia utoaji wa Tuzo za Oscar mwaka 2015.

Lupita ambaye ni mzaliwa wa Mexico, mwenye asili ya Kenya amejipatia jina kubwa miaka ya hivi karibuni katika tasnia ya filamu baada ya kushiriki filamu za 12 Years A Slave, Queen Of Katwe na Black Panther, zilizofanya vizuri zaidi kwenye tasnia hiyo. Mbali na mafanikio yake amekuwa akizungumza na mabinti ambao wanapigania ndoto zao pamoja na kinamama waliokata tamaa ili kuzifufua ndoto walizozika mioyoni mwao na kuamini kwamba siku moja watafanikiwa.

Lupita ambaye katika familia yake amezaliwa peke yake, mara kadhaa akizungumza na watu amekuwa akisema kwamba hakuna kitu ambacho anajivunia kwa sasa kama rangi yake ya mwili (kuwa mweusi). Hebu msikie hapa; “Wakati nimetangazwa kuwa nitakuwa miongoni mwa wazungumzaji katika Tuzo za Oscar nilipokea barua pepe kutoka kwa binti mmoja ambaye alikuwa ananipa ushuhuda kwamba, nimebadilisha maisha yake.” Anasema Lupita katika mahojiano yake na Jarida la Vogue na kuendelea:

Binti huyo aliniambia kwamba kwa muda mrefu alikuwa akihangaika kutumia vipodozi ili ngozi yake iweze kung’aa. Alikuwa anachukia kuwa mweusi na kila mara alikuwa akimwambia Mungu amfanyie miujiza siku moja alale na kuamka amebadilika. “Jambo la kushangaza kadiri alivyoendelea kutumia vipodozi ndivyo alivyoendelea kuwa mweusi. Lakini baada ya kunifahamu, kuona dunia ilivyonipokea na heshima niliyonayo, binti huyu ameamua kuamini katika rangi yake na kumshukuru Mungu.”

Anaendelea kuwa suala la kukutana na mabinti na kuelezwa kwamba wanachukia kuwa weusi ni jambo ambalo amekutana nalo kila mara. Lakini amekuwa akiwaambia kama bibi yake alivyomwambia. Uzuri hauliwi na hauwezi kumletea mtu mabadiliko katika maisha yake, zaidi ya kukubali vile alivyo. Lupita amewahi kueleza pia katika mahojiano na Jarida la Essense kwamba uzuri ni kitu ambacho kila mtu anatakiwa kuwa nacho. Vile ulivyo ndiyo uzuri wako na unatakiwa kujikubali kabisa.

Ukijiamini vile ulivyo na kujiona wewe ni mzuri kuliko wanawake wengine wote duniani, unaweza kufanya makubwa na kuwa yeyote yule ambaye unahitaji kuwa duniani. Hivyo ndivyo Lupita anavyoamini na anapenda kila mwanamke kuamini hivyo kama kama kweli anataka kuishi maisha ya furaha na kutimiza ndoto zake. Lakini pia Lupita mara kwa mara amekuwa akihamasisha kwamba wanawake wasijiwekee ‘limit’ katika suala zima la kuota, kwani hata yeye kabla ya kuwa staa hakuwa akiwaza kuwa muigizaji.

Ndoto zangu kubwa zilikuwa ni kusoma na kufanya kazi kwenye nyumba za masaji. Napenda sana kufanya masaji. Lakini baadaye nilijikuta nimekuwa muigizaji ninayeangaliwa na dunia. “Kwa hiyo kikubwa mwanamke yeyote duniani anatakiwa asijiwekee mipaka katika kuota na kuhangaika. Fanya lolote lile unaloamini litakufikisha kwenye mafanikio yako,” anamaliza Lupita Nyong’o.

LUPITA NYONG’O NI NANI? Jina lake kamili ni Lupita Amondi Nyong’o, amezaliwa mwaka 1983. Ni mtoto wa mwanasiasa maarufu nchini Kenya, Peter Anyang’ Nyong’o. Amezaliwa Mexico ambako baba yake alikuwa akifundisha lakini akaja kukulia na kusoma Kenya. Baadaye alikwenda katika Chuo cha Hampshire nchini Marekani ambako alichukua Shahada ya Sanaa na Uigizaji.

Baada ya hapo alianza kazi ya uigizaji Hollywood mwaka 2008, akafanya kazi nyingi ambazo zilimfanya ang’are duniani kote na kuwa Lupita mwingine kabisa tofauti na yule ambaye watu walikuwa wakimcheka na kumsimanga kwa weusi wake. Makala: Boniphace Ngumije