USHINDI WA RAIS UHURU KENYATTA WAPINGWA MAHAKAMANI

Bofya Hapa

 

Nairobi, Kenya. Mbunge wa zamani na mfanyabiashara maarufu John Mwau na muungano wa wanaharakati uitwao Kura Yangu Sauti Yangu, Jumatatu walifungua kesi Mahakama ya Juu kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta alioupata kwenye uchaguzi wa marudio Oktoba 26.
Aliyekuwa wa kwanza kufungua kesi alikuwa Mwau anayetaka Mahakama ya Juu kubatilisha uchaguzi huo wa marudio ulioitishwa baada ya mahakama hiyo hiyo kuweka historia kwa kuufuta ule wa Agosti 8 na kuamuru ufanyike mwingine katika muda wa siku 60.
Mbunge huyo wa zamani anapinga katika kesi hiyo kujumuishwa kwenye uchaguzi huo mgombea ambaye ametangazwa na mahakama kuwa amefilisika na kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) ilipaswa kusimamia upya mchakato wa uteuzi wa kupitisha wagombea urais, kama hukumu ilivyosema.
Baadaye wanaharakati wa Kura Yangu Sauti Yangu walifungua pia kesi kupinga ushindi wa Kenyatta katika uchaguzi ambao mpinzani wake mkuu wa National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga alisusia
Odinga alikuwa kiini cha ushindi wa Kenyatta kufutwa baada ya kufungua kesi Mahakama ya Juu akilalamikia dosari kadhaa na ukiukwaji wa Katiba uliofanywa na IEBC. Katika uchaguzi wa awali Kenyatta alishinda kwa asilimia 54 lakini wa marudio alijikusanyia asilimia 98 huku walioshiriki wakipungua hadi kuwa asilimia 38.8.